Sala ya kujikinga na maadui
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Utenzi wa Daudi wakati mtu mmoja kutoka Zifu alipomwendea Shauli na kumjulisha kuwa Daudi amejificha kwao.)
1 Uniokoe, ee Mungu, kwa jina lako;
unitetee kwa nguvu yako.
2 Uisikie, ee Mungu, sala yangu;
uyategee sikio maneno ya kinywa changu.
3 Watu wenye kiburi wananishambulia;
wakatili wanayawinda maisha yangu,
watu ambao hawamjali Mungu.
4 Najua Mungu ni msaada wangu,
Mwenyezi-Mungu hutegemeza maisha yangu.
5 Yeye atawaadhibu maadui zangu kwa uovu wao wenyewe;
kwa uaminifu wako, ee Mungu, uwaangamize.
6 Nitakutolea tambiko kwa moyo mkunjufu;
nitakushukuru kwa kuwa ni vema.
7 Maana umeniokoa katika taabu zangu zote,
nami nimewaona maadui zangu wameshindwa.