Kumtumainia Mungu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Njiwa Mkimya wa Mbali”. Utenzi wa Daudi baada ya kukamatwa na Wafilisti kule Gathi)
1 Ee Mungu, unionee huruma,
maana watu wananishambulia.
Mchana kutwa maadui wananidhulumu.
2 Mchana kutwa maadui zangu wananishambulia;
ni wengi mno hao wanaonipiga vita.
3 Ee Mungu Mkuu, hofu inaponishika,
mimi nakutumainia wewe.
4 Namtumainia Mungu na kusifu neno lake;
namtumainia Mungu, wala siogopi.
Binadamu dhaifu atanifanya nini?
5 Mchana kutwa wanapotosha kisa changu;
mawazo yao yote ni ya kunidhuru.
6 Wanakutana kupanga na kunivizia;
wanachunguza yote nifanyayo;
wananiotea kwa shabaha ya kuniua.
7 Ee Mungu, uwalipe kwa kadiri ya uovu wao,
uwaangushe hao waovu kwa hasira yako.
8 Wewe wakujua kusukwasukwa kwangu;
waweka kumbukumbu ya machozi yangu yote.
Je, yote si yamo kitabuni mwako?
9 Kila mara ninapokuomba msaada wako,
maadui zangu wanarudishwa nyuma.
Najua kweli Mungu yuko upande wangu.
10 Namtumaini Mungu na kusifu neno lake;
namtumainia Mwenyezi-Mungu na kusifu neno lake.
11 Namtumainia Mungu, wala siogopi.
Binadamu atanifanya nini?
12 Ee Mungu, nitatimiza ahadi zangu kwako;
nitakutolea tambiko za shukrani,
13 Maana umeniokoa katika kifo,
naam, umenilinda nisianguke chini;
nipate kuishi mbele yako, ee Mungu,
katika mwanga wa uhai.