Mungu hakimu wa mahakimu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi)
1 Enyi watawala,je, mwahukumu kwa haki kweli?
Je, mnawahukumu watu kwa adili?
2 La! Nyinyi mwafikiria tu kutenda maovu;
nyinyi wenyewe mwaeneza dhuluma nchini.
3 Waovu wamepotoka tangu kuzaliwa kwao,
waongo hao, wamekosa tangu walipozaliwa.
4 Wana sumu kama sumu ya nyoka;
viziwi kama joka lizibalo masikio,
5 ambalo halisikii hata sauti ya mlozi,
au utenzi wa mganga stadi wa uchawi.
6 Ee Mungu, wavunje meno yao,
yangoe, ee Mwenyezi-Mungu, meno ya simba hao.
7 Watoweke kama maji yanayodidimia mchangani,
kama nyasi wakanyagwe na kunyauka,
8 watoweke kama konokono ayeyukavyo,
kama mimba iliyoharibika isiyoona kamwe jua!
9 Kabla hawajatambua, wangolewe
kama miiba, michongoma au magugu.
Kwa hasira ya Mungu, wapeperushwe mbali,
wakiwa bado hai.
10 Waadilifu watafurahi waonapo waovu wanaadhibiwa;
watatembea katika damu ya watu wabaya.
11 Watu wote watasema: “Naam, waadilifu hupata tuzo!
Hakika yuko Mungu anayeihukumu dunia!”