Kuomba ulinzi
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mungu, usikie kilio changu,
usikilize sala yangu.
2 Ninakulilia kutoka miisho ya dunia,
nikiwa nimevunjika moyo.
Uniongoze juu kwenye mwamba mkubwa
3 maana wewe ndiwe kimbilio langu,
kinga yangu imara dhidi ya adui.
4 Naomba nikae nyumbani mwako milele
nipate usalama chini ya mabawa yako.
5 Ee Mungu, umezisikia ahadi zangu,
umenijalia sehemu yangu unayowapa wale wakuchao.
6 Umjalie mfalme maisha marefu,
miaka yake iwe ya vizazi vingi.
7 Atawale milele mbele yako, ee Mungu;
fadhili na uaminifu wako vimlinde.
8 Hivyo nitakuimbia nyimbo za sifa,
nikizitekeleza ahadi zangu kila siku.