Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
(Zaburi ya Daudi wakati alipokuwa katika jangwa la Yudea)
1 Ee Mungu, wewe u Mungu wangu,
nami nakutafuta kwa moyo;
roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu;
nina kiu kama nchi kavu isiyo na maji.
2 Nimetaka kukuona patakatifuni pako,
niione nguvu yako na utukufu wako.
3 Fadhili zako ni bora kuliko maisha,
nami nitakusifu kwa mdomo wangu.
4 Nitakushukuru maisha yangu yote;
nitainua mikono yangu na kukuomba.
5 Roho yangu inafurahi kama kwa karamu na vinono;
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
6 Niwapo kitandani ninakukumbuka,
usiku kucha ninakufikiria;
7 maana wewe umenisaidia daima.
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
8 Roho yangu inaambatana nawe kabisa,
mkono wako wa kulia wanitegemeza.
9 Lakini hao wanaotaka kuyaangamiza maisha yangu,
watatumbukia chini kwenye makao ya wafu.
10 Watauawa kwa upanga,
watakuwa chakula cha mbweha.
11 Lakini mfalme atafurahi kwa sababu ya Mungu;
wanaoahidi kwa jina la Mungu watamsifu,
lakini vinywa vya waongo vitafumbwa.