Sala ya kuomba ulinzi wa Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Usikie, ee Mungu, lalamiko langu;
yalinde maisha yangu na vitisho vya maadui.
2 Unikinge na njama za waovu,
na ghasia za watu wabaya.
3 Wananoa ndimi zao kama upanga,
wanafyatua maneno ya ukatili kama mishale.
4 Toka mafichoni wamshambulia mtu mnyofu,
wanamshambulia ghafla bila kuogopa.
5 Wanashirikiana katika nia yao mbaya;
wanapatana mahali pa kuficha mitego yao.
Wanafikiri: “Hakuna atakayeweza kuiona.”
6 Hufanya njama zao na kusema:
“Sasa tumekamilisha mpango!
Nani atagundua hila zetu?”
Mipango ya siri imefichika moyoni mwa mtu!
7 Lakini Mungu atawapiga mishale,
na kuwajeruhi ghafla.
8 Atawaangamiza kwa sababu ya maneno yao;
kila atakayewaona atatikisa kichwa.
9 Hapo watu wote wataogopa;
watatangaza aliyotenda Mungu,
na kufikiri juu ya matendo yake.
10 Waadilifu watafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu,
na kukimbilia usalama kwake;
watu wote wanyofu wataona fahari.