Kuomba msaada
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi ya matoleo ya ukumbusho)
1 Upende kuniokoa ee Mungu!
Ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia.
2 Wanaonuia kuniangamiza,
na waaibike na kufedheheka!
Hao wanaotamani niumie,
na warudi nyuma na kuaibika.
3 Hao wanaonisimanga,
na wapumbazike kwa kushindwa kwao.
4 Lakini wote wale wanaokutafuta,
wafurahi na kushangilia kwa sababu yako.
Wapendao wokovu wako,
waseme daima: “Mungu ni mkuu!”
5 Nami niliye maskini na fukara,
unijie haraka, ee Mungu!
Ndiwe msaada wangu na mkombozi wangu;
ee Mwenyezi-Mungu, usikawie!