Maombi kwa ajili ya taifa
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yungiyungi. Zaburi ya Asafu)
1 Utege sikio, ewe Mchungaji wa Israeli,
uwaongozaye wazawa wa Yosefu kama kondoo.
Ewe ukaaye juu ya viumbe vyenye mabawa,uangaze,
2 mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase.
Uoneshe nguvu yako, uje kutuokoa!
3 Uturekebishe, ee Mungu;
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.
4 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi,
hata lini utazikasirikia sala za watu wako?
5 Umefanya huzuni iwe chakula chetu;
umetunywesha machozi kwa wingi.
6 Umetufanya tuwe dharau kwa jirani zetu;
maadui zetu wanatudhihaki.
7 Ee Mungu wa majeshi, uturekebishe,
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.
8 Ulileta mzabibu kutoka Misri;
ukawafukuza watu wa mataifa mengine,
na kuupanda katika nchi yao.
9 Uliupalilia upate kukua,
nao ukatoa mizizi na kuenea kote nchini.
10 Uliifunika milima kwa kivuli chake,
na matawi yake yakawa kama mierezi mikubwa.
11 Matawi yake yalienea mpaka baharini;
machipukizi yake mpaka kando ya mto Eufrate.
12 Mbona ulibomoa kuta zilizouzunguka?
Sasa kila apitaye anachuma zabibu zake;
13 nguruwe mwitu wanauharibu,
na wanyama wa porini wanautafuna!
14 Utugeukie tena ee Mungu wa majeshi.
Uangalie toka mbinguni, uone;
ukautunze mzabibu huo.
15 Uulinde mche ulioupanda kwa mkono wako;
hilo chipukizi uliloimarisha wewe mwenyewe.
16 Watu walioukata na kuuteketeza,
uwatazame kwa ukali, waangamie.
17 Mkono wako umkinge huyo uliyemfadhili;
huyo uliyemteua kwa ajili yako.
18 Hatutakuacha na kukuasi tena;
utujalie uhai, nasi tutakusifu.
19 Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi uturekebishe;
utuangalie kwa wema, nasi tutaokoka.