Wimbo wa sikukuu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Gitithi. Zaburi ya Asafu)
1 Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu,
mshangilieni Mungu wa Yakobo;
2 vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma,
chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri.
3 Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo,
na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu.
4 Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli;
hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo.
5 Aliwapa watu wa Israeli agizo hilo,
alipoishambulia nchi ya Misri.
Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema:
6 “Mimi nilikutua mizigo yako mabegani,
nilikuondolea matofali uliyochukua mikononi.
7 Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa.
Nilikujibu nikiwa mafichoni katika ngurumo.
Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba.
8 Enyi watu wangu, sikieni onyo langu.
Laiti ungenisikiliza, ee Israeli!
9 Asiwepo kwako mungu wa kigeni;
usiabudu kamwe mungu mwingine.
10 Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,
niliyekutoa katika nchi ya Misri.
Fumbua kinywa chako, nami nitakulisha.
11 “Lakini watu wangu hawakunisikiliza;
Israeli hakunitaka kabisa.
12 Hivyo, nikawaacha wabaki na ukaidi wao;
wafuate mashauri yao wenyewe.
13 Laiti watu wangu wangenisikiliza!
Laiti Israeli angefuata njia yangu!
14 Ningewashinda maadui zao haraka;
ningenyosha mkono dhidi ya wadhalimu wao.
15 Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu,
na adhabu yao ingekuwa ya milele.
16 Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora,
ningekushibisha kwa asali ya mwambani.”