Kuliombea fanaka taifa
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Wakorahi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu,
umeifadhili nchi yako;
umemjalia Yakobo bahati nzuri tena.
2 Umewasamehe watu wako kosa lao;
umezifuta dhambi zao zote.
3 Umeizuia ghadhabu yako yote;
umeiacha hasira yako kali.
4 Uturekebishe tena, ee Mungu mwokozi wetu;
uiondoe chuki uliyo nayo juu yetu.
5 Je, utatukasirikia hata milele?
Je, utadumisha ghadhabu yako kwa vizazi vyote?
6 Je, hutatujalia tena maisha mapya,
ili watu wako wafurahi kwa sababu yako?
7 Utuoneshe, fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu,
utujalie wokovu wako.
8 Hebu nisikie anachosema Mwenyezi-Mungu;
maana anaahidi kuwapa watu wake amani,
watu wake mwenyewe wasiporudia upuuzi wao
9 Hakika yu tayari kuwaokoa wanaomheshimu,
na utukufu wake utadumu nchini mwetu.
10 Fadhili zake na uaminifu vitakutana;
uadilifu na amani vitaungana.
11 Uaminifu utachipuka katika nchi;
uadilifu utashuka toka mbinguni.
12 Naam, Mwenyezi-Mungu atatuletea fanaka,
na nchi yetu itatoa mazao yake mengi.
13 Uadilifu utamtangulia Mungu
na kumtayarishia njia yake.