Sifa ya Yerusalemu
(Zaburi ya Wakorahi. Wimbo)
1 Mungu amejenga mji wake
juu ya mlima wake mtakatifu.
2 Mwenyezi-Mungu anaupenda mji wa Siyoni,
kuliko makao mengine ya Yakobo.
3 Mambo ya fahari yanasemwa juu yako, ee mji wa Mungu:
4 “Miongoni mwa wale wanijuao mimi,
wapo watu wa Misrina Babuloni.
Kadhalika Filistia, Tiro na Kushi,
wote walizaliwa kwako!”
5 Na kuhusu Siyoni itasemwa:
“Siyoni ni mama wa huyu na huyu;
Mungu Mkuu atauthibitisha.”
6 Mwenyezi-Mungu ataandika katika kitabu,
atakapoorodhesha watu:
“Huyu amezaliwa huko!”
7 Wote wanacheza ngoma na kuimba:
“Siyoni, chanzo chetu ni kwako.”