Wimbo wa kumsifu Mungu
(Zaburi. Wimbo wa siku ya Sabato)
1 Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu,
kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu.
2 Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi,
na uaminifu wako nyakati za usiku,
3 kwa muziki wa zeze na kinubi,
kwa sauti tamu ya zeze.
4 Ee Mwenyezi-Mungu, matendo yako yanifurahisha;
nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda.
5 Matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, ni makuu mno!
Mawazo yako ni mazito mno!
6 Mtu mpumbavu hawezi kufahamu,
wala mjinga hajui jambo hili:
7 Kwamba waovu waweza kustawi kama nyasi,
watenda maovu wote waweza kufanikiwa,
lakini mwisho wao ni kuangamia milele,
8 bali wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u mkuu milele.
9 Hao maadui zako, ee Mwenyezi-Mungu,
naam, hao maadui zako, hakika wataangamia;
wote watendao maovu, watatawanyika!
10 Wewe umenipa nguvu kama nyati;
umenimiminia mafuta ya kuburudisha.
11 Kwa macho nimeona maadui zangu wameshindwa;
nimesikia kilio chao watendao maovu.
12 Waadilifu hustawi kama mitende;
hukua kama mierezi ya Lebanoni!
13 Kama miti iliyopandwa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu,
hustawi katika nyua za Mungu wetu;
14 huendelea kuzaa matunda hata uzeeni;
daima wamejaa utomvu na wabichi;
15 wapate kutangaza kwamba Mwenyezi-Mungu ni mnyofu,
Mwamba wangu, kwake hamna upotovu.