Utenzi wa kumsifu Mungu
1 Njoni tumwimbie Mwenyezi-Mungu,
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
2 Twende mbele zake na shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa.
3 Maana Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mkuu;
yeye ni Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Vilindi vyote vya dunia vimo mikononi mwake,
vilele vya milima ni vyake.
5 Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
kwa mikono yake aliiumba nchi kavu.
6 Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mwenyezi-Mungu, Muumba wetu!
7 Maana yeye ni Mungu wetu,
nasi ni watu wa kundi lake,
ni kondoo wake anaowachunga.
Laiti leo mngesikiliza sauti yake:
8 “Msiwe wakaidi kama kule Meriba,
kama walivyokuwa kule Masa jangwani,
9 wazee wenu waliponijaribu na kunipima,
ingawa walikuwa wameona mambo niliyowatendea.
10 Kwa miaka arubaini nilichukizwa nao,
nikasema: ‘Kweli, hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa njia zangu!’
11 Basi, nilikasirika, nikaapa:
‘Hawataingia mahali pangu pa pumziko!’”