Mungu mtawala mkuu
1 Mwenyezi-Mungu anatawala!
Furahi, ee dunia!
Furahini enyi visiwa vingi!
2 Mawingu na giza nene vyamzunguka;
uadilifu na haki ni msingi wa utawala wake.
3 Moto watangulia mbele yake,
na kuwateketeza maadui zake pande zote.
4 Umeme wake wauangaza ulimwengu;
dunia yauona na kutetemeka.
5 Milima yayeyuka kama nta mbele ya Mwenyezi-Mungu;
naam, mbele ya Bwana wa dunia yote.
6 Mbingu zatangaza uadilifu wake;
na mataifa yote yauona utukufu wake.
7 Wote wanaoabudu sanamu wanaaibishwa,
naam, wote wanaojisifia miungu duni;
miungu yote husujudu mbele zake.
8 Watu wa Siyoni wanafurahi;
watu wa Yuda wanashangilia,
kwa sababu ya hukumu zako, ee Mungu.
9 Wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu juu ya dunia yote;
wewe watukuka juu ya miungu yote.
10 Mwenyezi-Mungu huwapenda wanaochukia uovu,
huyalinda maisha ya watu wake;
huwaokoa makuchani mwa waovu.
11 Mwanga humwangazia mtu mwadilifu,
na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
12 Furahini kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu;
mshukuruni kwa ajili ya jina lake takatifu.