Mungu mtawala wa dunia yote
1 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya,
kwa maana ametenda mambo ya ajabu!
Mkono wake hodari, mkono wake mtakatifu umempatia ushindi.
2 Mwenyezi-Mungu ameonesha ushindi wake;
ameyadhihirishia mataifa uwezo wake wa kuokoa.
3 Amekumbuka fadhili na uaminifu wake kwa Waisraeli.
Pande zote za dunia zimeuona ushindi wa Mungu wetu.
4 Dunia yote imshangilie Mwenyezi-Mungu;
imsifu kwa nyimbo na vigelegele.
5 Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa shangwe,
msifuni kwa sauti tamu za zeze.
6 Mpigieni vigelegele Mwenyezi-Mungu mfalme wetu,
mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu.
7 Bahari na ivume na vyote vilivyomo;
dunia na wote waishio ndani yake.
8 Enyi mito pigeni makofi;
enyi vilima imbeni pamoja kwa shangwe.
9 Shangilieni mbele ya Mwenyezi-Mungu,
maana anakuja kutawala dunia.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
atawatawala watu kwa uadilifu.