Mungu mtawala mkuu
1 Mwenyezi-Mungu anatawala,
mataifa yanatetemeka!
Ameketi juu ya viumbe vyenye mabawa,
nayo dunia inatikisika!
2 Mwenyezi-Mungu ni mkuu katika Siyoni;
ametukuka juu ya mataifa yote.
3 Wote na walisifu jina lake kuu la kutisha.
Mtakatifu ndiye yeye!
4 Ee mfalme mkuu, mpenda uadilifu!
Umethibitisha haki katika Israeli;
umeleta uadilifu na haki.
5 Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu;
angukeni kifudifudi mbele zake.
Mtakatifu ndiye yeye!
6 Mose na Aroni walikuwa makuhani wake;
Samueli alikuwa miongoni mwa waliomlilia.
Walimlilia Mwenyezi-Mungu naye akawasikiliza.
7 Alisema nao katika mnara wa wingu;
waliyazingatia matakwa yake na amri alizowapa.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wewe uliwasikiliza;
kwao ulikuwa Mungu mwenye kusamehe,
ingawa uliwaadhibu kwa makosa yao.
9 Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu;
abuduni katika mlima wake mtakatifu!
Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.