1 “Siku hiyo, kutatokea chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi wazawa wa Daudi na wakazi wote wa Yerusalemu.
2 Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, majina ya vinyago vya miungu nchini nitayaondoa, wala hayatakumbukwa tena. Na wanaojidai kuwa manabii nitawaondolea mbali pamoja na tamaa zao za kuabudu sanamu.
3 Mtu yeyote akijidai kuwa nabii, baba na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Unapaswa kufa kwa kuwa unasema uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu’. Na haohao wazazi wake watamchoma kisu akiwa anatabiri.
4 Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu,
5 bali kila mmoja atasema, ‘Mimi si nabii. Mimi ni mkulima tu; nimeimiliki ardhi tangu ujana wangu’.
6 Na mtu akimwuliza mmoja wao, ‘Vidonda hivi ulivyo navyo mgongoni vimetoka wapi?’ Yeye atajibu, ‘Vidonda hivi nilivipata katika nyumba ya rafiki zangu.’”
7 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:
“Amka, ee upanga!
Inuka umshambulie mchungaji wangu;
naam, mchungaji anayenitumikia.
Mpige mchungaji na kondoo watawanyike.
Nitaunyosha mkono wangu,
kuwashambulia watu wadhaifu.
8 Theluthi mbili za watu katika nchi zitaangamizwa;
ni theluthi moja tu itakayosalimika.
9 Theluthi hiyo moja itakayosalia,
nitaijaribu na kuitakasa,
kama mtu asafishavyo fedha,
naam, kama ijaribiwavyo dhahabu.
Hapo wao wataniomba mimi,
nami nitawajibu.
Nitasema, ‘Hawa ni watu wangu’,
nao watasema, ‘Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu.’”