Yerusalemu baada ya kuangamia
1 Jinsi gani dhahabu yetu ilivyochujuka,
dhahabu safi kabisa ilivyobadilika!
Mawe ya thamani yametawanywa
yamesambaa barabarani kote.
2 Watoto wa Siyoni waliosifika sana,
waliothaminiwa kama dhahabu safi,
jinsi gani sasa wamekuwa kama vyombo vya udongo,
kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3 Hata mbwamwitu huwa na hisia za mama
na kuwanyonyesha watoto wao;
lakini watu wangu wamekuwa wakatili,
hufanya kama mbuni nyikani.
4 Midomo ya watoto wachanga imekauka kwa kiu,
watoto wanaomba chakula lakini hakuna anayewapa.
5 Watu waliojilisha vyakula vinono
sasa wanakufa njaa barabarani.
Waliolelewa na kuvikwa kifalme
sasa wanafukua kwa mikono kwenye majaa.
6 Watu wangu wamepata adhabu kubwa
kuliko watu wa mji wa Sodoma
mji ambao uliteketezwa ghafla
bila kuwa na muda wa kunyosha mkono.
7 Vijana wa Siyoni walikuwa safi kuliko theluji,
walikuwa weupe kuliko maziwa.
Miili yao ilikuwa myekundu kama matumbawe,
uzuri wa viwiliwili vyao kama johari ya rangi ya samawati.
8 Sasa sura zao ni nyeusi kuliko makaa,
wanapita barabarani bila kujulikana;
ngozi yao imegandamana na mifupa yao
imekauka, imekuwa kama kuni.
9 Afadhali waliouawa kwa upanga
kuliko waliokufa kwa njaa,
ambao walikufa polepole
kwa kukosa chakula.
10 Kina mama ambao huwa na huruma kuu
waliwapika watoto wao wenyewe,
wakawafanya kuwa chakula chao
wakati watu wangu walipoangamizwa.
11 Mwenyezi-Mungu alionesha uzito wa ghadhabu yake,
aliimimina hasira yake kali;
aliwasha moto huko mjini Siyoni
ambao uliteketeza misingi yake.
12 Wafalme duniani hawakuamini
wala wakazi wowote wa ulimwenguni,
kwamba mvamizi au adui
angeweza kuingia malango ya Yerusalemu.
13 Hayo yalisababishwa na dhambi za manabii wake,
yalitukia kwa sababu ya uovu wa makuhani wake
ambao walimwaga damu ya waadilifu mjini kwake.
14 Walitangatanga barabarani kama vipofu,
walikuwa wamekuwa najisi kwa damu,
hata asiwepo mtu yeyote wa kuwagusa.
15 Watu waliwapigia kelele wakisema:
“Tokeni, nendeni zenu enyi mlio najisi!
Tokeni, tokeni, msiguse chochote.”
Hivyo wakawa wakimbizi na kutangatanga;
watu wa mataifa walitamka:
“Hawa hawatakaribishwa kukaa kwetu!”
16 Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwatawanya,
wala hatawajali tena.
Makuhani hawatapata tena heshima,
wazee hawatapendelewa tena.
17 Tulichoka kukaa macho kungojea msaada;
tulikesha na kungojea kwa hamu
taifa ambalo halikuweza kutuokoa.
18 Watu walifuatilia hatua zetu,
tukashindwa kupita katika barabara zetu.
Siku zetu zikawa zimetimia;
mwisho wetu ukawa umefika.
19 Waliotufuatia walikuwa wepesi kuliko tai,
walitukimbiza milimani,
walituvizia huko nyikani.
20 Walimnasa yule ambaye maisha yetu yalimtegemea,
yule mfalme aliyewekwa wakfu wa Mwenyezi-Mungu,
yule ambaye tulisema: “Chini ya ulinzi wake
tutaishi miongoni mwa mataifa.”
21 Wakazi wa Edomu, mwaweza kushangilia kwa sasa,
mwaweza kwa sasa kufurahi enyi wakazi wa Uzi;
lakini kikombe hiki cha adhabu kitawajia pia,
nanyi pia mtakinywa na kulewa,
hata mtayavua mavazi yenu!
22 Adhabu ya uovu wako ewe Siyoni imekamilika;
Mwenyezi-Mungu hatawaacha zaidi uhamishoni.
Lakini nyinyi Waedomu atawaadhibu kwa uovu wenu,
atazifichua dhambi zenu.