Yeremia 45

Ahadi ya Mungu kwa Baruku

1 Haya ndiyo maneno aliyotamka nabii Yeremia mnamo mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia naye Baruku mwana wa Neria akawa anayaandika kitabuni.

Yeremia alimwambia Baruku:

2 “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi juu yako wewe Baruku:

3 Wewe ulisema, ‘Ole wangu! Mwenyezi-Mungu ameniongezea uchungu juu ya maumivu yangu. Nimechoka kupiga kite, wala sipati pumziko.’

4 Lakini Mwenyezi-Mungu ameniambia nikuambie hivi: Tazama, yale niliyojenga nayabomoa, na yale niliyopanda nayangoa; nitafanya hivyo katika nchi yote.

5 Je, wewe unajitakia mambo makubwamakubwa? Usiyatafute! Achana nayo, maana, ninaleta maangamizi juu ya wanadamu wote. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wewe tuzo lako ni hili: Nitayaokoa maisha yako kila mahali utakapokwenda.”