Wimbo wa shukrani
1 Siku hiyo mtasema:
“Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu,
maana ingawa ulinikasirikia,
hasira yako imetulia,
nawe umenifariji.
2 Mungu ndiye mwenye kuniokoa,
nitamtegemea yeye, wala sitaogopa;
Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu;
yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.”
3 Mtachota maji kwa furaha
kutoka visima vya wokovu.
4 Siku hiyo mtasema:
“Mshukuruni Mwenyezi-Mungu
mwombeni kwa jina lake.
Yajulisheni mataifa matendo yake,
tangazeni kuwa jina lake limetukuka.
5 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa
kwa kuwa ametenda mambo makuu;
haya na yajulikane duniani kote.
6 Pazeni sauti na kuimba kwa furaha,
enyi wakazi wa Siyoni,
maana aliye mkuu miongoni mwenu
ndiye Mungu, Mtakatifu wa Israeli.”