Zaburi 148

Ulimwengu wote umsifu Mungu

1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka mbinguni,

msifuni kutoka huko juu mbinguni.

2 Msifuni, enyi malaika wake wote,

msifuni, enyi majeshi yake yote.

3 Msifuni, enyi jua na mwezi,

msifuni, enyi nyota zote zingaazo.

4 Msifuni, enyi mbingu za juu,

na maji yaliyo juu ya mbingu.

5 Vyote vilisifu jina la Mwenyezi-Mungu,

maana yeye aliamuru, na vyote vikawa.

6 Yeye aliviweka mahali pao daima,

kwa amri ambayo haiwezi kubatilishwa.

7 Msifuni Mwenyezi-Mungu kutoka duniani;

enyi majoka ya baharini na vilindini, msifuni.

8 Msifuni enyi moto, mvua ya mawe na theluji,

upepo wa tufani unaotimiza amri yake!

9 Msifuni enyi milima na vilima,

miti ya matunda na misitu!

10 Msifuni enyi wanyama wa porini na wafugwao,

viumbe vitambaavyo na ndege wote!

11 Msifuni enyi wafalme na mataifa yote;

viongozi na watawala wote duniani!

12 Msifuni enyi wavulana na wasichana;

wazee wote na watoto pia!

13 Nyote lisifuni jina la Mwenyezi-Mungu,

maana jina lake peke yake latukuka;

utukufu wake wapita dunia na mbingu.

14 Amewapa watu wake nguvu;

heshima kwa watu wote waaminifu,

watu wa Israeli wapenzi wake.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!