Sala ya shukrani
1 Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kwa moyo wangu wote,
naimba sifa zako mbele ya miungu.
2 Ninasujudu kuelekea hekalu lako takatifu;
nalisifu jina lako,
kwa sababu ya fadhili zako na uaminifu wako;
kwa sababu umeweka jina lako na neno lako
juu ya kila kitu.
3 Nilipokulilia, wewe ulinijibu;
umeniongezea nguvu zangu.
4 Wafalme wote duniani watakusifu, ee Mwenyezi-Mungu,
kwa sababu wameyasikia maneno yako.
5 Wataimba sifa za matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu,
kwa maana utukufu wako ni mkuu.
6 Ingawa wewe ee Mwenyezi-Mungu, uko juu ya wote,
unawaangalia kwa wema walio wanyonge;
nao wenye kiburi huwaona kutoka mbali.
7 Hata nikikumbana na taabu, wewe wanilinda;
waunyosha mkono wako dhidi ya hasira ya maadui zangu wakali;
kwa nguvu yako kuu wanisalimisha.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, utatimiza yote uliyoniahidi.
Fadhili zako, ee Mwenyezi-Mungu, zadumu milele.
Usisahau kazi ya mkono wako mwenyewe.