Ombolezo ugenini
1 Kando ya mito ya Babuloni, tulikaa,
tukawa tunalia tulipokumbuka Siyoni.
2 Katika miti ya nchi ile,
tulitundika zeze zetu.
3 Waliotuteka walitutaka tuwaimbie;
watesi wetu walitutaka tuwafurahishe:
“Tuimbieni mojawapo ya nyimbo za Siyoni!”
4 Twawezaje kuimba wimbo wa Mwenyezi-Mungu
katika nchi ya kigeni?
5 Ee Yerusalemu, kama nikikusahau,
mkono wangu wa kulia na ukauke!
6 Ulimi wangu na uwe mzito,
kama nisipokukumbuka wewe, ee Yerusalemu;
naam, nisipokuthamini kuliko furaha yangu kubwa!
7 Ee Mwenyezi-Mungu, usisahau waliyotenda Waedomu,
siku ile Yerusalemu ilipotekwa;
kumbuka waliyosema:
“Bomoeni mji wa Yerusalemu!
Ngoeni hata na misingi yake!”
8 Ee Babuloni, utaangamizwa!
Heri yule atakayekulipiza mabaya uliyotutenda!
9 Heri yule atakayewatwaa watoto wako
na kuwapondaponda mwambani!