Zaburi 133

Uzuri wa umoja kati ya watu

(Wimbo wa Kwenda Juu, wa Daudi)

1 Ni jambo zuri na la kupendeza sana

ndugu kuishi pamoja kwa umoja.

2 Ni kama mafuta mazuri yatiririkayo kichwani,

mpaka kwenye ndevu zake Aroni,

mpaka upindoni mwa vazi lake shingoni.

3 Ni kama umande wa mlima Hermoni,

uangukao juu ya vilima vya Siyoni!

Huko Mwenyezi-Mungu ameahidi kuwabariki watu wake,

kuwapa uhai usio na mwisho.