Tuzo kwa jamaa imchayo Mungu
(Wimbo wa Kwenda Juu)
1 Heri wote wamchao Mwenyezi-Mungu,
wanaoishi kufuatana na amri zake.
2 Utapata matunda ya jasho lako,
utafurahi na kupata fanaka.
3 Mkeo atakuwa kama mzabibu wa matunda mengi nyumbani mwako;
watoto wako kama chipukizi za mzeituni kuzunguka meza yako.
4 Naam, ndivyo atakavyobarikiwa
mtu amchaye Mwenyezi-Mungu.
5 Mwenyezi-Mungu akubariki kutoka Siyoni!
Uione fanaka ya Yerusalemu, siku zote za maisha yako.
6 Uishi na hata uwaone wajukuu zako!
Amani iwe na Israeli!