Kuomba msaada
(Wimbo wa Kwenda Juu
)
1 Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu,
naye akanijibu.
2 Uniokoe ee Mwenyezi-Mungu,
na watu wadanganyifu na waongo.
3 Enyi watu wadanganyifu, mtapewa kitu gani?
Mtaadhibiwa namna gani?
4 Kwa mishale mikali ya askari,
kwa makaa ya moto mkali!
5 Ole wangu kwamba naishi kama mgeni huko Mesheki;
naishi kama mgeni katika mahema ya Kedari.
6 Nimeishi muda mrefu mno
kati ya watu wanaochukia amani!
7 Wakati ninaposema nataka amani,
wao wanataka tu vita.