Zaburi 112

Furaha ya mtu mwema

1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Heri mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu,

anayefurahia sana kutii amri zake.

2 Wazawa wake watakuwa wenye nguvu nchini;

watoto wa wanyofu watapata baraka.

3 Nyumbani kwake kutakuwa na mali nyingi;

uadilifu wake wadumu milele.

4 Mtu mwema huangaziwa mwanga gizani;

mtu mwenye huruma, mpole na mwadilifu.

5 Mtu mkarimu akopeshaye bila faida, hufanikiwa;

mtu afanyaye shughuli zake kwa kutumia haki.

6 Mwadilifu hatashindwa kamwe,

huyo atakumbukwa milele.

7 Hana haja ya kuogopa akipata habari mbaya;

ana moyo thabiti na humtegemea Mwenyezi-Mungu.

8 Yuko imara moyoni, wala hataogopa;

naye atawaona maadui zake wanashindwa.

9 Hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini;

uadilifu wake wadumu milele.

Nguvu yake inatukuzwa kwa heshima.

10 Watu waovu huona hayo na kuudhika;

husaga meno kwa chuki na kutoweka,

matazamio ya mtu mbaya huishia patupu.