Mungu asifika kwa matendo yake
1 Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Nitamshukuru Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote,
nikijumuika na jamii ya watu waadilifu.
2 Matendo ya Mwenyezi-Mungu ni makuu mno!
Wote wanaoyafurahia huyatafakari.
3 Kila afanyacho kimejaa utukufu na fahari;
uadilifu wake wadumu milele.
4 Amesababisha matendo yake ya ajabu yakumbukwe;
Mwenyezi-Mungu ni mwema na mwenye huruma.
5 Huwapa chakula wenye kumcha;
hasahau kamwe agano lake.
6 Amewaonesha watu wake nguvu ya matendo yake,
amewapa nchi za mataifa mengine ziwe mali yao.
7 Matendo yake ni ya haki na ya kuaminika;
kanuni zake zote ni za kutegemewa.
8 Amri zake zadumu daima na milele;
zimetolewa kwa haki na uadilifu.
9 Aliwakomboa watu wake
na kufanya nao agano la milele.
Yeye ni mtakatifu na wa kutisha mno!
10 Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima;
wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara.
Sifa zake zadumu milele.