Kuomba msaada
(Sala ya Daudi)
1 Unitegee sikio, ee Mwenyezi-Mungu, unijibu,
maana mimi ni fukara na mnyonge.
2 Uyahifadhi maisha yangu maana mimi ni mchaji wako;
uniokoe mimi mtumishi wako ninayekutegemea.
3 Wewe ni Mungu wangu;
basi, unionee huruma,
maana nakulilia mchana kutwa.
4 Uifurahishe roho yangu mimi mtumishi wako,
maana sala zangu nazielekeza kwako ee Bwana.
5 Wewe, ee Bwana, u mwema na mwenye kusamehe;
mwingi wa fadhili kwa wote wakuombao.
6 Ee Mwenyezi-Mungu, uitegee sikio sala yangu;
ukisikie kilio cha ombi langu.
7 Siku za taabu nakuita,
maana wewe waniitikia.
8 Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe;
hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe.
9 Mataifa yote uliyoyaumba, yatakuja kukuabudu, ee Bwana;
yatatangaza ukuu wa jina lako.
10 Wewe ndiwe mkuu, wafanya maajabu;
wewe peke yako ndiwe Mungu.
11 Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu,
nipate kuwa mwaminifu kwako;
uongoze moyo wangu nikuheshimu.
12 Ee Bwana, Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wote;
nitatangaza ukuu wa jina lako milele.
13 Fadhili zako kwangu ni nyingi mno!
Umeniokoa kutoka chini kuzimu.
14 Ee Mungu, watu wenye kiburi wamenikabili;
kundi la watu wakatili wanataka kuniua,
wala hawakujali wewe hata kidogo.
15 Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa rehema na huruma;
wewe ni mvumilivu, mwingi wa fadhili na uaminifu.
16 Unigeukie, unihurumie;
unijalie nguvu yako mimi mtumishi wako,
umwokoe mtoto wa mjakazi wako.
17 Unioneshe ishara ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu,
ili wale wanaonichukia waaibike,
waonapo umenisaidia na kunifariji.