Hamu ya kuwa nyumbani kwa Mungu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Gitithi. Zaburi ya Wakorahi)
1 Jinsi gani yanavyopendeza makao yako,
ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi!
2 Nafsi yangu yatamani mno maskani ya Mwenyezi-Mungu!
Moyo na mwili wangu wote wamshangilia Mungu aliye hai.
3 Hata shomoro wamepata makao yao,
mbayuwayu wamejenga viota vyao,
humo wameweka makinda yao,
katika madhabahu zako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu!
4 Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,
wakiimba daima sifa zako.
5 Heri watu wanaopata nguvu zao kwako,
wanaotamani kwenda kuhiji mlimani kwako.
6 Wapitapo katika bonde kavu la Baka,
hulifanya kuwa mahali pa chemchemi,
na mvua za vuli hulijaza madimbwi.
7 Wanaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi;
watamwona Mungu wa miungu huko Siyoni.
8 Usikie sala yangu ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi;
unitegee sikio, ee Mungu wa Yakobo.
9 Ee Mungu, umwangalie kwa wema ngao yetu mfalme,
umtazame huyo uliyemweka wakfu kwa mafuta.
10 Siku moja tu katika maskani yako,
ni bora kuliko siku elfu mahali pengine;
afadhali kusimama mlangoni pa nyumba yako,
kuliko kuishi nyumbani kwa watu waovu.
11 Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu;
yeye hutuneemesha na kutujalia fahari.
Hawanyimi chochote kilicho chema,
wale waishio kwa unyofu.
12 Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi,
heri mtu yule anayekutumainia wewe!