Mungu mtawala mkuu
(Zaburi ya Asafu)
1 Mungu anasimamia baraza lake;
anatoa hukumu katika kusanyiko la miungu:
2 “Mpaka lini mtaendelea kuhukumu bila haki
na kuwapendelea watu waovu?
3 Wapeni wanyonge na yatima haki zao;
tekelezeni haki za wanaoonewa na fukara.
4 Waokoeni wanyonge na maskini,
waokoeni makuchani mwa wadhalimu.
5 “Lakini nyinyi hamjui wala hamfahamu!
Nyinyi mnatembea katika giza la upotovu!
Misingi yote ya haki duniani imetikiswa!
6 Mimi nilisema kuwa nyinyi ni miungu;
kwamba nyote ni watoto wa Mungu Mkuu!
7 Hata hivyo, mtakufa kama watu wote;
mtaanguka kama mkuu yeyote.”
8 Inuka ee Mungu, uuhukumu ulimwengu;
maana mataifa yote ni mali yako.