Mungu mshindi
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Asafu. Wimbo)
1 Mungu anajulikana katika Yuda;
jina lake ni kuu katika Israeli.
2 Makao yake yamo huko Salemu;
maskani yake huko Siyoni.
3 Huko alivunja mishale ya adui;
alivunja ngao, panga na silaha za vita.
4 Wewe, ee Mungu, watukuka mno;
umejaa fahari kuliko milima ya milele.
5 Wenye nguvu walipokonywa nyara zao,
sasa wamelala usingizi wa kifo,
mashujaa wa vita hawakuweza kutumia mikono yao.
6 Ulipowakemea, ee Mungu wa Yakobo,
farasi na wapandafarasi walikufa ganzi.
7 Wewe, ee Mungu, ni wa kutisha mno!
Nani awezaye kustahimili mbele yako ukikasirika?
8 Ulijulisha hukumu yako toka mbinguni;
dunia iliogopa na kunyamaza;
9 wakati ulipoinuka kutekeleza hukumu,
kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani.
10 Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako;
na waliookoka vitani watafanya sikukuu zako.
11 Mtimizieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ahadi zenu;
enyi mlio karibu mpeni zawadi Mungu wa kutisha.
12 Yeye huzitoa roho za wakuu;
huwatisha wafalme wa dunia.