Mungu hakimu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu”. Zaburi ya Asafu. Wimbo)
1 Tunakushukuru, ee Mungu,
tunakushukuru!
Tunatangaza ukuu wa jina lako
na kusimulia juu ya matendo yako makuu.
2 Mungu asema: “Mimi nimeweka wakati maalumu!
Wakati huo nitahukumu kwa haki.
3 Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo,
mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake.
4 Nawaambia wenye kiburi:
‘Acheni kujigamba’;
na waovu: ‘Msioteshe pembe za kiburi!
5 Msijione kuwa watu wa maana sana,
wala kusema maneno ya majivuno.’”
6 Hukumu haitoki mashariki au magharibi;
wala haitoki nyikani au mlimani.
7 Mungu mwenyewe ndiye hakimu;
humshusha mmoja na kumkweza mwingine.
8 Mwenyezi-Mungu, anashika kikombe mkononi,
kimejaa divai kali ya hasira yake;
anaimimina na waovu wote wanainywa;
naam, wanainywa mpaka tone la mwisho.
9 Lakini mimi nitafurahi milele,
nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo.
10 Atavunja nguvu zote za watu waovu;
lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha.