Zaburi 67

Wimbo wa shukrani

(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi. Wimbo)

1 Utuonee huruma, ee Mungu, utubariki;

utuelekezee uso wako kwa wema;

2 dunia yote ipate kutambua njia yako,

mataifa yote yajue nguvu yako ya kuokoa.

3 Watu wote wakutukuze, ee Mungu;

watu wote na wakusifu!

4 Mataifa yote yafurahi na kuimba kwa furaha;

maana wawahukumu watu kwa haki,

na kuyaongoza mataifa duniani.

5 Watu wote wakutukuze, ee Mungu;

watu wote na wakusifu!

6 Nchi imetoa mazao yake;

Mungu, Mungu wetu, ametubariki.

7 Mungu aendelee kutubariki.

Watu wote duniani na wamche.