Mungu mlinzi wangu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi)
1 Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu,
kwake watoka wokovu wangu.
2 Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu,
yeye ni ngome yangu, sitatikisika.
3 Hata lini mtanishambulia mimi?
Hata lini nyinyi nyote mtanipiga,
mimi niliye kama kiambaza kilichoinama,
kama ukuta unaoanza kubomoka?
4 Mmepanga kuniangusha toka mahali pangu pa heshima;
furaha yenu ni kusema uongo.
Kwa maneno, mnabariki,
lakini moyoni mnalaani.
5 Namngojea Mungu peke yake kwa utulivu;
kwake naliweka tumaini langu.
6 Yeye peke yake ndiye mwamba na wokovu wangu,
yeye ni ngome yangu, sitatikisika.
7 Wokovu na fahari yangu vyatoka kwa Mungu;
mwamba wangu mkuu na kimbilio langu ni Mungu.
8 Enyi watu, mtumainieni Mungu daima;
mfungulieni Bwana yaliyo moyoni mwenu.
Mungu ndiye kimbilio la usalama wetu.
9 Binadamu wote ni kama pumzi tu;
wote, wakubwa kwa wadogo, hawafai kitu.
Tena ukiwapima uzito hawafikii kilo,
wote pamoja ni wepesi kuliko pumzi.
10 Msitegemee dhuluma,
msijisifie mali ya wizi;
kama mali zikiongezeka, msizitegemee.
11 Mungu ametamka mara moja,
nami nimesikia tena na tena:
Kwamba enzi ni mali yake Mungu;
12 naam, nazo fadhili ni zake Bwana;
humlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.