Kuomba msaada
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi alipomponyoka Shauli na kujificha pangoni)
1 Unihurumie, ee Mungu, unihurumie,
maana kwako nakimbilia usalama.
Kivulini mwa mabawa yako nitakimbilia usalama,
hata hapo dhoruba ya maangamizi itakapopita.
2 Namlilia Mungu Mkuu,
Mungu anikamilishiaye nia yake.
3 Atanipelekea msaada toka mbinguni na kuniokoa;
atawaaibisha hao wanaonishambulia.
Mungu atanionesha fadhili zake na uaminifu wake!
4 Mimi nimezungukwa na maadui,
wenye uchu wa damu kama simba;
meno yao ni kama mikuki na mishale,
ndimi zao ni kama panga kali.
5 Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu!
Utukufu wako uenee duniani kote!
6 Maadui wamenitegea wavu waninase,
nami nasononeka kwa huzuni.
Wamenichimbia shimo njiani mwangu,
lakini wao wenyewe wametumbukia humo.
7 Niko thabiti moyoni, ee Mungu,
naam, niko thabiti moyoni;
nitaimba na kukushangilia!
8 Amka, ee nafsi yangu!
Amkeni, enyi kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko!
9 Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;
nitakuimbia sifa kati ya mataifa.
10 Fadhili zako zaenea hata juu ya mbingu,
uaminifu wako wafika hata mawinguni.
11 Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu!
Utukufu wako uenee duniani kote!