Mtu asiyemcha Mungu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Mahalathi. Utenzi wa Daudi)
1 Wapumbavu hujisemea moyoni:
“Hakuna Mungu!”
Wote wamepotoka kabisa,
wametenda mambo ya kuchukiza;
hakuna hata mmoja atendaye jema.
2 Mungu anawaangalia wanadamu kutoka mbinguni,
aone kama kuna yeyote mwenye busara,
kama kuna yeyote anayemtafuta Mungu.
3 Lakini wote wamekosa,
wote wamepotoka pamoja,
hakuna atendaye mema,
hakuna hata mmoja.
4 “Je, hao watendao maovu hawana akili?
Wanawatafuna watu wangu kama mikate;
wala hawanijali mimi Mungu!”
5 Hapo watashikwa na hofu kubwa,
hofu ambayo hawajapata kuiona;
maana Mungu ataitawanya mifupa ya adui,
hao wataaibika maana Mungu amewakataa.
6 Laiti ukombozi wa Israeli ungefika kutoka Siyoni!
Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake,
wazawa wa Yakobo watashangilia;
Waisraeli watafurahi.