Hukumu ya Mungu
(Kwa Mwimbishaji. Utenzi wa Daudi baada ya Doegi, Mwedomu, kumwendea Shauli na kumjulisha kuwa Daudi amekwenda nyumbani kwa Abimeleki)
1 Mbona, ewe jitu, wajivunia ubaya wako
dhidi ya wenye kumcha Mungu?
2 Kila wakati unawaza maangamizi;
ulimi wako ni kama wembe mkali!
Unafikiria tu kutenda mabaya.
3 Wewe wapenda uovu kuliko wema,
wapenda uongo kuliko ukweli.
4 Ewe mdanganyifu mkuu,
wapenda mambo ya kuangamiza wengine.
5 Kwa hivyo Mungu atakuangamiza milele,
atakunyakua na kukuondoa nyumbani mwako;
atakungoa katika nchi ya walio hai.
6 Waadilifu wataona hayo na kuogopa,
kisha watakucheka na kusema:
7 “Tazameni yaliyompata mtu huyu!
Yeye hakutaka Mungu awe kimbilio lake;
bali alitegemea wingi wa mali yake,
na kutafuta humo usalama wake!”
8 Lakini mimi ni kama mzeituni mbichi,
unaostawi katika nyumba ya Mungu.
Nazitegemea fadhili zake milele na milele.
9 Ee Mungu, nitakushukuru daima,
kwa ajili ya mambo uliyofanya.
Nitatangaza kwamba wewe ni mwema,
mbele ya watu wako waaminifu.