Sala ya mgonjwa
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Heri mtu anayewajali maskini;
Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida.
2 Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai,
naye atafanikiwa katika nchi;
Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake.
3 Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa,
atamponya maradhi yake yote.
4 Nami nilisema: “Unifadhili, ee Mwenyezi-Mungu,
unihurumie maana nimekukosea wewe.”
5 Madui zangu husema vibaya juu yangu:
“Atakufa lini na jina lake litoweke!”
6 Wanitembeleapo husema maneno matupu;
wanakusanya mabaya juu yangu,
na wafikapo nje huwatangazia wengine.
7 Wote wanichukiao hunongonezana juu yangu;
wananiwazia mabaya ya kunidhuru.
8 Husema: “Maradhi haya yatamuua;
hatatoka tena kitandani mwake!”
9 Hata rafiki yangu wa moyoni niliyemwamini,
rafiki ambaye alishiriki chakula changu,
amegeuka kunishambulia!
10 Ee Mwenyezi-Mungu, unionee huruma!
Unipe nafuu, nami nitawalipiza.
11 Hivyo nitajua kwamba unapendezwa nami,
maadui zangu wasipopata fahari juu yangu.
12 Wewe umenitegemeza kwani natenda mema;
waniweka mbele yako milele.
13 Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele!
Amina! Amina!