Sala katika mateso
(Zaburi ya Daudi ya matoleo)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako;
usiniadhibu kwa ghadhabu yako.
2 Mishale yako imenichoma;
mkono wako umenigandamiza.
3 Hamna mahali nafuu mwilini mwangu,
kwa sababu umenikasirikia;
hamna penye afya hata mifupani mwangu,
kwa sababu ya dhambi yangu.
4 Nimefunikwa kabisa na dhambi zangu,
zinanilemea kama mzigo mzito mno kwangu.
5 Madonda yangu yameoza na kunuka,
na hayo ni matokeo ya ujinga wangu.
6 Nimepindika mpaka chini na kupondeka;
mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
7 Viungo vyangu vimeshambuliwa na homa;
mwilini mwangu hamna nafuu yoyote.
8 Nimelegea na kupondekapondeka;
nasononeka kwa kusongwa moyoni.
9 Ee Bwana, wewe wajua tazamio langu lote;
kwako hakikufichika kilio changu.
10 Moyo wanidunda, nguvu zimeniishia;
hata macho yangu nayo yamekwisha fifia.
11 Rafiki na wenzangu wanaepa kuona mateso yangu,
na jamaa zangu wanakaa mbali nami.
12 Wanaotaka kuniua wanatega mitego yao;
wanaonitakia niumie wanatishia kuniangamiza.
Mchana kutwa wanafanya mipango dhidi yangu.
13 Lakini mimi nimekuwa kama kiziwi, sisikii;
nimekuwa kama bubu asiyeweza kusema kitu.
14 Naam, nimekuwa kama mtu asiyesikia,
kama mtu asiye na chochote cha kujitetea.
15 Lakini ninakutumainia wewe, ee Mwenyezi-Mungu;
wewe, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, ndiwe utakayenijibu.
16 Nakuomba tu maadui wasinisimange,
wasione fahari juu ya kuanguka kwangu.
17 Karibu sana nitaanguka;
nakabiliwa na maumivu ya daima.
18 Naungama uovu wangu;
dhambi zangu zanisikitisha.
19 Maadui zangu hawajambo, wana nguvu;
ni wengi mno hao wanaonichukia bure.
20 Hao wanaonilipa maovu kwa wema wangu,
wananipinga kwa sababu natenda mema.
21 Usinitupe, ee Mwenyezi-Mungu;
ee Mungu wangu, usikae mbali nami.
22 Uje haraka kunisaidia;
ewe Mwenyezi-Mungu, uliye wokovu wangu.