Zaburi 36

Uovu wa binadamu

(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu)

1 Dhambi huongea na mtu mwovu,

ndani kabisa moyoni mwake;

jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake.

2 Mwovu hujipendelea mwenyewe,

hufikiri uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa.

3 Kila asemacho ni uovu na uongo;

ameacha kutumia hekima na kutenda mema.

4 Alalapo huwaza kutenda maovu,

hujiweka katika njia isiyo njema,

wala haachani na uovu.

Wema wa Mungu

5 Fadhili zako ee Mwenyezi-Mungu zaenea hata mbinguni;

uaminifu wako wafika mawinguni.

6 Uadilifu wako ni kama milima mikubwa,

hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.

Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama

7 Jinsi gani zilivyo bora fadhili zako!

Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.

8 Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;

wawanywesha kutoka mto wa wema wako.

9 Wewe ndiwe asili ya uhai;

kwa mwanga wako twaona mwanga.

10 Uendelee kuwafadhili wale wanaokutambua;

uzidi kuwa mwema kwa wanyofu wa moyo.

11 Usikubali wenye majivuno wanivamie,

wala watu waovu wanikimbize.

12 Kumbe watendao maovu wameanguka;

wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.