Maondoleo ya dhambi
(Zaburi ya Daudi. Funzo)
1 Heri yake mtu aliyesamehewa kosa lake,
mtu ambaye dhambi yake imeondolewa kabisa.
2 Heri mtu ambaye Mwenyezi-Mungu hamwekei hatia,
mtu ambaye hana hila moyoni mwake.
3 Wakati nilipokuwa sijakiri dhambi yangu,
nilikuwa nimedhoofika kwa kulia mchana kutwa.
4 Mchana na usiku mkono wako ulinilemea;
nikafyonzwa nguvu zangu,
kama maji wakati wa kiangazi.
5 Kisha nilikiri makosa yangu kwako;
wala sikuuficha uovu wangu.
Nilisema ninakuungamia makosa yangu ee Mwenyezi-Mungu,
ndipo nawe ukanisamehe dhambi zangu zote.
6 Kwa hiyo, kila mwaminifu na akuletee maombi;
jeshi likaribiapo au mafuriko,
hayo hayatamfikia yeye.
7 Wewe ndiwe kinga yangu;
wewe wanilinda katika taabu.
Umenijalia shangwe za kukombolewa.
8 Mungu asema: “Nitakufunza
na kukuonesha njia unayopaswa kufuata.
Nitakushauri kwa uangalifu mkubwa.
9 Usiwe mpumbavu kama farasi au nyumbu,
ambao lazima wafungwe lijamu na hatamu,
la sivyo hawatakukaribia.”
10 Watu waovu watapata mateso mengi,
bali wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu wazungukwa na fadhili zake.
11 Furahini na kushangilia kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu;
pigeni vigelegele vya shangwe enyi wanyofu wa moyo.