Kuomba msaada
(Zaburi ya Daudi)
1 Nakulilia, ee Mwenyezi-Mungu!
Ewe mwamba wa usalama wangu usiniwie kama kiziwi,
la sivyo kama usiponisikiliza,
nitakuwa kama wale washukao shimoni kwa wafu.
2 Sikiliza sauti ya ombi langu,
ninapokulilia unisaidie,
ninapoinua mikono yangu kuelekea maskani yako takatifu.
3 Usinipatilize pamoja na watu wabaya,
pamoja na watu watendao maovu:
Watu wasemao na wenzao maneno ya amani,
kumbe wamejaa uhasama moyoni.
4 Uwaadhibu kadiri ya matendo yao,
kufuatana na maovu waliyotenda.
Waadhibu kadiri ya matendo yao wenyewe;
uwatendee yale wanayostahili.
5 Hawajali matendo ya Mwenyezi-Mungu;
hawatambui mambo aliyoyafanya.
Kwa sababu hiyo atawabomoa,
wala hatawajenga tena upya.
6 Atukuzwe Mwenyezi-Mungu,
maana amesikiliza ombi langu.
7 Mwenyezi-Mungu ndiye nguvu yangu na ngao yangu;
tegemeo la moyo wangu limo kwake.
Amenisaidia nami nikashangilia kwa moyo;
kwa wimbo wangu ninamshukuru.
8 Mwenyezi-Mungu ni nguvu ya watu wake;
yeye ni kimbilio la wokovu kwa mfalme wake mteule.
9 Ee Mungu, uwaokoe watu wako;
uwabariki watu hao walio mali yako.
Uwe mchungaji wao na kuwategemeza milele.