Kwa Mungu kuna usalama
(Zaburi ya Daudi)
1 Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu na wokovu wangu,
ni nani nitakayemwogopa?
Mwenyezi-Mungu ni ngome ya maisha yangu,
sitamwogopa mtu yeyote.
2 Waovu wakinishambulia,
na kutaka kuniangamiza,
hao wapinzani wangu watajikwaa na kuanguka.
3 Hata jeshi likinizunguka,
moyo wangu hautaogopa kitu;
hata nikikabiliwa na vita,
bado nitakuwa na tumaini.
4 Jambo moja nimemwomba Mwenyezi-Mungu,
nalo ndilo ninalolitafuta:
Nikae nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu
siku zote za maisha yangu;
niuone uzuri wake Mwenyezi-Mungu,
na kutafuta maongozi yake hekaluni mwake.
5 Siku ya taabu atanificha bandani mwake;
atanificha katika hema lake,
na kunisalimisha juu ya mwamba.
6 Nami kwa fahari nitaangalia juu
ya maadui zangu wanaonizunguka.
Nitamtolea tambiko kwa shangwe hekaluni mwake,
nitaimba na kumshangilia Mwenyezi-Mungu.
Msaada wapatikana kwa Mungu
7 Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia,
unionee huruma na kunijibu.
8 Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!”
Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu.
9 Usiache kuniangalia kwa wema.
Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako;
wewe umekuwa daima msaada wangu.
Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu.
10 Hata kama wazazi wangu wakinitupa,
Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake.
11 Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu;
uniongoze katika njia iliyo sawa,
kwa sababu ya maadui zangu.
12 Usiniache maadui wanitende wapendavyo;
maana mashahidi wa uongo wananikabili,
nao wanatoa vitisho vya ukatili.
13 Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu
katika makao ya walio hai.
14 Mtegemee Mwenyezi-Mungu!
Uwe na moyo, usikate tamaa!
Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!