Mungu mchungaji wangu
(Zaburi ya Daudi)
1 Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu,
sitapungukiwa na kitu.
2 Hunipumzisha kwenye malisho mabichi;
huniongoza kando ya maji matulivu,
3 na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya.
Huniongoza katika njia sawa
kwa hisani yake.
4 Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo,
sitaogopa hatari yoyote,
maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami;
gongo lako na fimbo yako vyanilinda.
5 Umeniandalia karamu mbele ya maadui zangu;
umenipaka mafuta kichwani pangu;
kikombe changu umekijaza mpaka kufurika.
6 Kweli wema wako na fadhili zako zitakuwa pamoja nami,
siku zote za maisha yangu;
nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu milele.