Kuomba ushindi
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni;
jina la Mungu wa Yakobo likulinde.
2 Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake;
akutegemeze kutoka mlima Siyoni.
3 Azikumbuke sadaka zako zote;
azikubali tambiko zako za kuteketezwa.
4 Akujalie unayotamani moyoni mwako,
aifanikishe mipango yako yote.
5 Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako;
tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu.
Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote!
6 Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua,
atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni;
kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa.
7 Wengine hujigamba kwa magari ya vita;
wengine hujigamba kwa farasi wao.
Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
8 Hao watajikwaa na kuanguka;
lakini sisi tutainuka na kusimama imara.
9 Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu;
utujibu wakati tunapokuomba.