Uovu wa watu
(Kwa Mwimbishaji. Zaburi ya Daudi)
1 Wapumbavu hujisemea moyoni:
“Hakuna Mungu.”
Wote wamepotoka kabisa,
wametenda mambo ya kuchukiza;
hakuna hata mmoja atendaye jema!
2 Mwenyezi-Mungu anawaangalia wanadamu kutoka mbinguni,
aone kama kuna yeyote mwenye busara,
kama kuna yeyote anayemtafuta Mungu.
3 Lakini wote wamekosa,
wote wamepotoka pamoja;
hakuna atendaye mema,
hakuna hata mmoja.
4 “Je, hao watendao maovu hawana akili?
Wanawatafuna watu wangu kama mikate;
wala hawanijali mimi Mwenyezi-Mungu.”
5 Hapo watashikwa na hofu kubwa,
maana Mungu yu pamoja na waadilifu.
6 Unaweza kuvuruga mipango ya maskini,
lakini Mwenyezi-Mungu ndiye kimbilio lake.
7 Laiti ukombozi wa Israeli ungefika kutoka Siyoni!
Mwenyezi-Mungu atakaporekebisha hali ya watu wake,
wazawa wa Yakobo watashangilia;
Waisraeli watafurahi.