Utukufu wa Mungu na cheo cha binadamu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Gitithi. Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wetu,
kweli jina lako latukuka duniani kote!
Utukufu wako waenea mpaka juu ya mbingu!
2 Kwa sifa za watoto wadogo na wanyonyao,
umejiwekea ngome dhidi ya adui zako,
uwakomeshe waasi na wapinzani wako.
3 Nikiangalia mbingu, kazi ya vidole vyako,
mwezi na nyota ulizozisimika huko,
4 mtu ni nini, ee Mungu, hata umfikirie,
binadamu ni nini hata umjali?
5 Umemfanya awe karibu kama Mungu,
umemvika fahari na heshima.
6 Ulimpa madaraka juu ya kazi zako zote;
uliviweka viumbe vyote chini ya mamlaka yake:
7 Kondoo, ng’ombe, na wanyama wa porini;
8 ndege, samaki, na viumbe vyote vya baharini.
9 Ee Mwenyezi-Mungu, Bwana wetu,
kweli jina lako latukuka duniani kote!