Sala wakati wa taabu
(Kwa Mwimbishaji: Na ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa Sheminithi. Zaburi ya Daudi)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako;
usiniadhibu kwa ghadhabu yako.
2 Unihurumie, ee Mwenyezi-Mungu, nimeishiwa nguvu;
uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nataabika mpaka mifupani.
3 Ninahangaika sana rohoni mwangu.
Ee Mwenyezi-Mungu, utakawia mpaka lini?
4 Unigeukie, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe;
unisalimishe kwa sababu ya fadhili zako.
5 Huko kwa wafu hakuna anayekukumbuka;
huko kuzimu ni nani awezaye kukusifu?
6 Niko hoi kwa kilio cha uchungu;
kila usiku nalowesha kitanda changu kwa machozi;
kwa kulia kwangu naulowesha mto wangu.
7 Macho yangu yamechoka kwa huzuni;
yamefifia kwa kutaabishwa na adui.
8 Ondokeni kwangu enyi nyote watenda maovu!
Maana Mwenyezi-Mungu amesikia kilio changu.
9 Mwenyezi-Mungu amesikia ombi langu;
Mwenyezi-Mungu amekubali sala yangu.
10 Maadui zangu wote wataaibika na kufadhaika;
watarudi nyuma na kuaibishwa ghafla.