Kuomba msaada asubuhi
(Zaburi ya Daudi alipomkimbia Absalomu)
1 Ee Mwenyezi-Mungu, tazama walivyo wengi adui zangu,
ni wengi mno hao wanaonishambulia.
2 Wengi wanasema juu yangu,
“Hatapata msaada kwa Mungu.”
3 Lakini wewe ee Mwenyezi-Mungu u ngao yangu kila upande;
kwako napata fahari na ushindi wangu.
4 Nakulilia kwa sauti, ee Mungu,
nawe wanisikiliza kutoka mlima wako mtakatifu.
5 Nalala na kupata usingizi,
naamka tena maana wewe ee Mwenyezi-Mungu wanitegemeza.
6 Sitayaogopa maelfu ya watu,
wanaonizingira kila upande.
7 Uje ee Mwenyezi-Mungu!
Niokoe ee Mungu wangu!
Wewe wawavunja mataya maadui zangu wote;
wawavunja meno waovu wasinidhuru.
8 Mwenyezi-Mungu ndiwe uokoaye;
uwape baraka watu wako.